Illustrations by Moussa Kone

Bichiboi

by Troy Onyango

First published as “Beach Boy” in the University of East Anglia Postgraduate Creative Writing Anthology, 2019

Translated into Swahili by Mary Mukami
Share:
  • Download:
 

Narrated in Swahili by Mary Mukami.

Hatimaye, tunaamua kutembea kwenye ufukwe wa bahari tukinywa maji ya madafu yetu huku tukifikiria cha kusemezeana, huku maneno yakikaba kinywa. Jua linatua kwenye upeo wa macho, nusu likiwa limezama baharini, na maji yanaonekana kama kioevu kikali kilichotapakaa juu ya bahari lenyewe, yakibadilisha rangi tulivu ya bluu kwa rangi iliyokolea ya machungwa. Shakwe linapaa na kuchukua umbo la mviringo na baadaye kutawanyika na kuchukua umbo la pembe tatu na kisha tena kurudi katika mviringo. Milio ya shakwe inatawala hewani, na upepo unavuma kuelekea mashariki, huku ukikatiza wimbo wa ndege hao. Tunatembea kimyakimya, tukiwa tumetekwa na milio ya sauti zinazotuzingira, maneno yetu yakiwa yamenaswa kwenye koo zetu. Maji yanapiga ufukwe wa bahari kwa upole na miguu yetu inapasua kijeuri mchanga wa bahari wenye changarawe ndogo. Ananigeukia – jicho lake la kulia likiwa limeinama ili kuniangalia – kisha anauliza, ‘Ungali unanipenda?’

Nachukua muda kabla ya kujibu na kuvuta maji ya madafu kupitia mrija wangu na kuyameza kwa nguvu, kumeza maji hayo kwa ghafla kunafanya karibu yaninyonge. Nakohoa kidogo na kuvuta pumzi iliyojaa chumvi na inayonuka kama samaki aliyekufa. Ninashusha pumzi kwa sauti kubwa. Jibu langu lipo kichwani lakini siko tayari kulitamka. Ninasema. Sauti ninazozisikia zinameza jibu langu, na ninapogeuka kumwangalia, ninaona umbo lake leusi linaelea, na kuteremka kuelekea upande wa chini na mitende inayoyumbayumba na kukumbatiana kana kwamba inapiga sala kwa udi na uvumba. Nina hamu ya kupaaza sauti na kumuuliza, ‘Je, nikisema ndio, nitakuona tena?’

Dhamira yangu inaniambia jinsi anavyoniaga, itakuwa chanzo cha hadithi nyingine isiyo na kikomo.

Ninatupa ganda la dafu chini na bahari inaimeza pamoja na mrija. Ninapoachwa peke yangu, wazo la kurejea kwenye chumba changu hotelini linanijia, lakini ukimya wa chumba hicho hufanya niwaze kuhusu kifo na ngono kana kwamba vitu hivyo viwili vinalingana. Na kwa sababu Theo harudi kwangu tena – nafahamu, nafahamu – hakuna haja ya kurejea haraka. Nina uhakika nikirejea nitapata jumbe kutoka kwake akidai ninavyompigia simu kila wakati nikiwa Pwani nikiwa na madhumuni ya kujitosheleza kutumia mwili wake. Najua atanilaani na kuniita mbinafsi, lakini kama ilivyo desturi, nitamkumbusha kuwa katu huwa simlazimishi kuja. Isitoshe, nitamkumbusha kuwa yeye ndio huwa ananitumia jumbe kila mara kuniuliza nitakwenda lini Mombasa kumwona. Mazungumzo haya yanafanyika akilini mwangu na baadaye naamua kutembea kwenye ufukwe wa bahari, kuelekea upande wa chini ambako majahazi yanaonekana kuwangoja watalii wanaopania kushuhudia saa za mwisho mwisho za machweo ya jua.

Upepo unavuma na kuisalimu ngozi ya kichwa changu na ungo la shingo yangu. Nakipapasa kichwa changu kilichonyolewa kukisheheni upepo, ingawa mateso hayo yanaendelea. Naendelea kutembea. Karatasi jeusi linaonekana ndani ya maji, na korongo anatumbukia ili kuikamata kabla ya kugundua upumbavu alioudhihirisha, kisha anajaribu kuitapika kwenye bahari. Kundi la ndege wanaoimba wanakusanyika na kumviringa korongo huyo anayeendelea kunaswa na karatasi ile. Upepo unabadililisha mwelekeo na kuanza kupepea kuelekea kusini. Najifunika uso kujisheheni dhidi ya upepo huo, macho yangu yakiwa yamemkazia korongo huyo ambaye anang’ang’ana kujinasua kutoka kwenye mtego huo. Nafikiri kinachompata ndege huyo kinamfaa kwani amenaswa akijaribu kunyakua baadhi ya samaki kutoka kwenye bahari, lakini nasita na kufikiria kuwa, korongo huyo alikuwa mimi. Ghafla, ninajawa na huruma na dhiki kuu, moyo wangu unaghathabika kwa sababu ya hisia nzito zinazonijaa mwilini. Ningekuwa na uwezo, ningelipaa na kwenda kumnasua, lakini nabakia kusimama kwenye ufukwe wa bahari, maji yakichezea miguu yangu, najihisi mnyonge.

Kutoka kona ya jicho langu – hadi upande wa kushoto – Naona umbo la mwanaume mrefu kiasi kunishinda na mwenye kifua kikubwa kama jiwe akitembea akielekea kwangu. Nywele zake zimefungwa kwa matuta makubwa ya dredi siyo kimitindo lakini kwa sababu ya kupuuza kutengeneza. Suruali alilovaa lenye rangi ambayo haijakolea sana limekunjwa mpaka kwa magoti. Anatembea kwa madaha ya kupita kiasi katika sehemu ya kina kifupi cha bahari ambapo povu linaonekana likiinuka juu. Maji yanasafisha miguu yake na michanga kuichafua kwa wakati huo huo. Anasimama kando yangu na kufuata kivuli changu hadi anaponiona ingawa fikra zangu zimenirudisha kumtazama korongo ambaye kwa wakati huu anaonekana akianguka chini na kuchapachapa mbawa zake kivivu ukilinganisha na hapo awali. Anamnyooshea mkono korongo huyo na kuniuliza ikiwa namtazama. Ninatingisha kichwa kuitikia bila ya kumwangalia, kisha anasema kwa masikitiko kuwa, korongo huyo anaelekea kufa. Anachodhibitisha katika wimbo wake wa Kiswahili ni kuwa korongo huyo ameshakufa. Ninakumbuka mrija wangu ukielea majini, nahisi ni kama koo langu linabanwa, na miguu yangu inaisha nguvu na kuhisi maumivu, kwa sababu mimi pia nimechangia msiba huo. Ninamuuliza ana uhakika gani kuwa korongo huyo hatanusurika. Ananijibu kwa kunihakikishia kuwa, ‘Bahari inakufa na vitu vyote vilivyo ndani yake.’

Ninapiga ulimi, nashusha pumzi na kumgeukia ingawaje macho yangu yanalingana na kidevu chake. Ninagundua kuwa nywele zake za kifua zinafanana kama msitu wa Kongo kwa mtazamo wa juu. Ana sura yenye mvutio ambao niliupenda hapo awali katika umri wangu wa miaka ya arobaini hivi – kabla ya kukutana na Theo. Ninajaribu kuanza mazungumzo naye na kumwuliza yeye hujishughulisha na nini, lakini anapasua kicheko kinachosikika kama kohozi lililokauka.

‘Inaonekana wewe hutoki hapa karibu, ni kweli?’ Anauliza.

‘La, nimezuru. Natoka Nairobi.’

‘Ah, nilijua tu! ‘We ni wale wa Bara.’ Ananitania na kubadilisha lafudhi ambayao sijawahi kuisikia katu maishani, lakini ninajua hivyo ndivyo wakosti wanadhania watu kama mimi wanaotoka bara huzungumza.

Papo hapo ninaangaza macho yangu angani, namuona korongo akianguka na kutumbukia majini kwa kishindo kama kimondo. Sauti inayosikika ni hafifu na wala haikawii, lakini ninapoisikia, mwili wangu unajikunyata. Mawimbi ya maji yanayoonekana yanathibitisha aliyotabiri mtu huyu nisiyemjua yametendeka. Upepo umetulia. Ukimya unaotawala ni mkuu; ni kama kwamba dunia imekwisha pamoja na korongo huyo.

‘Watafuta nini huku?’

Sauti yake inanikumbusha bado yuko hapa, amesimama umbali wa inchi kadhaa kutoka kwangu, ngozi yake inanuka chumvi inayobaki baada ya kutoa jasho na maji yakuvukiza. Sauti ya kitoto anayotoa inanikumbusha mara ya kwanza nilipokutana na Theo kwenye klabu moja huko Lavington nilipommwagia kinywaji kwenye vazi lake leupe la kitani, akanitusi kuwa mimi ni mpumbavu na kuwa ninajibeba kiholela. Niliduwaa na kumwangalia akiendelea kunitusi huku nimenyamaza, na ingawa sikutarajia, kabla ya kumaliza usemi wake, aliacha matusi na baadaye akaomba msamaha. Nilimwahidi kumnunulia vinywaji vingine na kumpeleka dukani kumnunulia nguo zingine mpya siku iliyofuata. Hiyo ni karibu miaka kumi iliyopita na Theo, kijana mdogo, ambaye niliyemjua wakati huyo, aliyekosa subira, alikuwa mtu mwengine, mtu aliyenifahamu na aliyetambua jinsi ya kunipenda. Hangenikosea kimakusudi, hata siku ile aliponijulisha kuwa anahama Nairobi.

‘Huku hakukaliki,’ alisema – alipomaanisha, ‘Jiji hili haliridhishi moyo wangu.’

Nageuka na kumtazama mwanaume huyu nisiyemjua na kumwambia sitafuti chochote. Anaguna na kuniambia, ‘Sawa. Lakini ninachojua ni kuwa mtu yeyote anayekuja huku chini huwa anatafuta kitu.’ Mwanaume huyu anaonekana ni kama ameishi Pwani kwa muda mrefu kuliko ninavyomfikiria. Natabasamu na kumwuliza umri wake. Anachana nywele zake kutumia vidole vyake na kuniambia, ‘Una hakika hilo ndilo swali unalotaka kujua?’ Unaweza kuulizia bangi, kokeni, na wanawake wa kutomba mpaka uume wako ulegee, chochote kile na unaamua kuuliza umri wangu?’ ‘Kaka, una mchezo sana!’

Anacheka lakini kwa wakati huu kicheko kinasikika kuwa tofauti, ni kana kwamba kinatoka kwa mtu tofauti, ni kama Theo wa ujanani. Nina hamu ya kukichukua kicheko chake pindi tu anapomaliza kucheka, nikiweke mikononi mwangu na niishi nacho kwa muda mrefu. Anaendelea kucheka kana kwamba anafahamu kuwa kicheko chake kinavutia. Maji ni matulivu mno.

‘Sipendelei wanawake vile,’ ninamwambia, kisha ninainamisha kichwa changu kana kwamba usemi nilioukiri umenilemea. Sina hamu ya kuona namna ambavyo uso wake unabadilika hivyo naangalia kando, kwenye bahari, ambayo sasa imegeuka na kuwa nyeusi kana kwamba imetiwa sumu ya mauti.

‘Ha, ungesema hivyo,’ ananijibu, ‘Ninaweza kutafutia bichiboi kwa hela kidogo.’

Ninafikiria kuondoka hapo kabla ya kufanya makosa, lakini naamua kuendelea kusimama kusikia atakachopendekeza.

‘Unapenda wembamba ama wenye misuli?’ Anauliza.

Mtu angefikiri anazungumza kuhusu mnyama, anayeishi ili aliwe nyama tu.

‘Kama tu wewe,’ Namtania. Kama yeye.

‘Ah kaka, una hela ngapi?’

Ninawaza kuhusu kiwango chochote bila ya kufikiria, hela ambazo nitampatia kwa urahisi ikiwa ana uhakika ya tunayozungumzia.

‘Elfu ishirini, ‘Ninamjibu. Punde tu baada ya kutamka kiwango hicho ndipo nagundua ni kikubwa, lakini pesa hazina maana kubwa sana kwangu; nilirithi pesa hizi zote kutoka kwa baba yangu aliyejibidiisha kuhakikisha ningepata maisha bora zaidi. Vilevile, nilijitafutia riziki miaka mingi sana katika wizara ya fedha hivyo nilikuwa na uwezo wa kugharamia chochote nilichotaka. Huwa naamini kuwa maisha ni mafupi sana na ni muhimu kufurahia hela zako ulizozipata kupitia jasho lako. Haswa kwa wakati huu ambapo najihisi mzee na mara nyingi inakuwa vigumu kuvipata vitu hivi kwa urahisi. ‘Wallahi!’ anashangaa na kukubaliana na pendekezo langu na vilevile kuonyesha mshangao wa kutoamini. ‘Ndio.’ ‘Kaka, mimi nitakufira ukitaka.’ Maana mimi si shoga lakini hela ni hela.’

Mimi si shoga lakini hela ni hela – nayawaza maneno yake kichwani mwangu. Ninamwangalia na kujiuliza kwanini nilikataa kuhamia Pwani na Theo. Kwanini ninakubali kujilimbikizia upweke Nairobi ilhali nina Theo wangu, ambaye daima ana subira kwangu, ambaye daima ananipenda. Ninaskiza sauti tulivu ya bahari. Ninaskia nyimbo za shakwe kwa umbali. Na ukimya wa korongo aliye majini.

Lazima nimweleze Theo kuwa, ‘Bahari inakufa na vitu vyote vilivyo ndani yake.’

Natembea kwa haraka kuelekea hotelini mwangu. Kile ninachosikia ni sauti ya nyayo za mwanaume anayenifuata nyuma.